
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe
(Mb), Jana tarehe 03 Mei, 2017 amekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya
Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, jijini Mwanza. Mhe.
Mwakyembe alipokea hotuba na matamko kutoka kwa Mabalozi na wawakilishi
wa taasisi mbalimbali zikiwemo Umoja wa Mataifa, UNESCO, Umoja wa Nchi
za Ulaya, Baraza la Habari Tanzania, Mfuko wa Vyombo vya Habari na Klabu
za Waandishi wa Habari Mikoani.
Katika
hotuba yake, Mhe. Mwakyembe aliwahakikishia Wanahabari kwamba Serikali
itaendelea kuweka mazingira bora, salama na wezeshi ili kuilea na
kuikuza tasnia ya habari. Mhe. Mwakyembe amewakumbusha wanahabari kwamba
Serikali tayari ilishakamilisha utungaji wa Sheria ya Haki ya Kupata
Taarifa na Sheria ya Huduma za Habari ambazo zote zimekamilika mwaka
2016, hivyo wazizingatie katika utendaji kazi wao.
Mhe.
Mwakyembe pia aliwasihi wanahabari kuwa wakweli na kuzingatia misingi
na maadili katika kazi zao. "Mlinzi wa kwanza wa Waandishi wa Habari ni
Mungu, Mlinzi wa Pili ni Kalamu ya Mwandishi mwenyewe hasa anapozingatia
maadili ya kazi yake," alisisitiza Mhe. Mwakyembe. Mhe. Mwakyembe
alielekeza Idara ya Habari ya Habari-Maelezo kuwa na utaratibu wa
kukutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari mara kwa mara ili
kubadilishana mawazo na kutoa taarifa sahihi za Serikali.
Aidha,
Mhe. Mwakyembe aliwashauri wanahabari kuzichukulia taarifa za mitandao
ya kijamii kama "tetesi" ambazo huitaji utafiti kabla ya kuzitumia. Mhe.
Mwakyembe alivitaka vituo vyote vya runinga na redio viwe vinasoma
vichwa vya Habari tu vya magazeti na visisome habari hizo kwa kina mpaka
kurasa za ndani za magazeti kwa kufanya hivyo kunaathiri biashara za
magazeti.
Mhe.
Mwakyembe pia alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa hakuna uhuru usio na
mipaka hivyo wanahabari watimize wajibu wao bila husda wala mawaa na
kuzingatia misingi ya sheria na taaluma. Aidha, Mhe. Mwakyembe
amewaahidi wanahabari wote ushirikiano wa karibu kwa wakati wote na
ameweka utaratibu wa kukutana nao mara kwa mara ili kutazitatua
changamoto zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment